HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, February 5, 2016

JESHI LA POLISI KANDA MAALUMU YA DAR ES SALAAM LASITISHA ULINZI SHIRIKISHI MJINI.

Na Avila Kakingo, Globu ya Jamii.
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lasitisha shughuli za ulinzi shirikishi kwa muda usiojulikana katika vituo vya Polisi vya mjini kati kutokana na malalamiko na utendaji kazi ambao hauna tija kwa jamii.

Kauli hiyo imekuja baada ya kamanda wa polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam kuona mapungufu mbalimbali ikiwa na matendo yenye harufu ya rushwa, vikundi hivyo kutokufuata sheria na taratibu za ukamataji kwa kutumia nguvu kupita kiasi hata pale isipohitajika pamoja na utendaji mbovu.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.

Katazo hilo limesababisha kufungiwa kwa vikundi vya ulinzi shirikishi kwa muda usiojulikana  mpaka pale Jeshi la polisi litakapo lidhishwa na kuwapa mafunzo maalumu ya ukamataji wa bodaboda zinazovunja sheria za barabarani.

Pia Kamanda Sirro amesema kuwa limefanikiwa kukamata magari mawili yanayosadikiwa  kubeba vitu vilivyoibwa kwenye ofisi ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA)  magari hayo ni Toyota Noah yenye namba za usajili T 989 CNV  na Mitubish Pajero yenye namba za usajili T 386 CVV na kuwakamata walinzi wawili waliokuwa zamu kulinda siku hiyo katika jengo hilo.

"Katika wizi huo vitu vilivyoibwa ni Compyuta mbili, aina ya Dell pamoja na CPU, Monitor zake na Televisheni moja aina ya Sumsung inchi 40" Alisema Sirro.

Katika tukio jingine Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kuokoa Tumbaku boksi 71 yenye thamani ya shilingi 150,000,000 mali ya Ahmed Huwel miaka 36 mfanyabiashara na mkazi wa Msasani Regent.

Kamanda wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusiana na kukamatwa kwa magari mawili yaliyohusika katika wizi ofisi ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA)
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Kamanda wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro leo jijini Dar es Salaam.
Picha na Avila Kakingo wa Globu ya Jamii.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad