HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, December 19, 2014

AISHA MADINDA AZIKWA LEO,KIGAMBONI JIJINI DAR

WAKURUGENZI wa bendi hasimu za dansi Tanzania, African Stars, Asha Baraka na Extra Bongo, Ali Choki, leo wameongoza mamia ya waombolezaji kumzika aliyekuwa mnenguaji wa zamani wa bendi hizo, Aisha Mohamed Mbegu ‘Aisha Madinda’.

Mazishi ya Aisha Madinda yamefanyika leo kwenye Makaburi ya Kijiji cha Mikwambe, Kigamboni jijini Dar es Salaam, baada ya kukwama kufanyika jana kutokana na zuio la Jeshi la Polisi, kupisha uchunguzi wa sababu za kifo cha ghafla cha mnenguaji huyo.

Baada ya uchunguzi huo kufanyika na ripoti kukabidhiwa kwa Jeshi la Polisi na familia, mazishi hayo yakafanyika leo jioni yakihudhuriwa na Asha Baraka na Choki, pamoja na Makamu wa Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Salim Omari Mwinyi.

Akizungumza katika mazishi hayo, Asha Baraka ambaye ni Mkurugenzi wa African Stars Entertainment inayoimiliki Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’, alimuelezea Aisha kuwa ni sawa na mwanaye kutokana na muda mwingi aliotumia akiwa Twanga.

Baraka aliongeza kuwa licha ya kutokuwa na Aisha katika siku za karibuni, bado Twanga Pepeta inatambua na kuthamini mchango wa mkali huyo wa jukwaa na kwamba pengo lake halitasahaulika kirahisi ndani ya bendi hiyo kongwe.

Kwa upande wake Choki alisema daima atakumbuka uwajibikaji, usikivu na upendo wa Aisha akiwa na Extra Bongo ‘Wazee wa Kizigo,’ na kwamba kwake yeye marehemu ni sawa na dada yake, huku akimtaja kama mtumishi mwema.

“Alikuwa na Extra Bongo kwa muda mfupi, lakini aina yake ya utumishi utabaki katika kumbukumbu zetu daima. Huu ni mwaka wa taabu kwangu, kwani siku ya arobaini ya marehemu mke wangu, alifariki pia mzee wangu Shem Karenga,” alisikitika Choki.

Choki alienda mbali zaidi kwa kulalama kuwa, siku moja baada ya kumzika Shem Karenga, ndio siku aliyofariki Aisha Madinda, hivyo kuendeleza mfululizo wa majonzi kwake na wadau wa tasnia nzima ya muziki wa dansi nchini.

Kwa upande wake, mtoto wa dada wa marehemu, Sheikh Mohamed Mussa, ambaye aliongoza mazishi upande wa familia, aliwashukuru Watanzania kwa ushirikiano walioutoa katika kufanikisha mazishi hayo, huku akiwataka kuuendelea kumuombea.
 Mwili wa Aisha Madinda ukitolewa kwenye gari la kubebea maiti mara baada ya kuwasili nyumbani kwao,Kigamboni.
  Mwili wa Aisha Madinda ukiwasili nyumbani kwa ajili ya kuswaliwa kabla ya mazishi yaliyofanyika  katika makaburi ya Kibada, Kigamboni jijini Dar es salaam jioni hii.
 Mwili wa Aisha Madinda ukiswaliwa kabla ya maziko huko Kigamboni jijini Dar.
 Mwili wa Aisha Madinda ukipelekwa kwenye gari la kubebea maiti kwa ajili ya kwenda kwenye mazishi makaburi ya Kibada, Kigamboni.
Baadhi ya waombolezaji wakiwa kwenye msiba wa marehemu  Aisha Madinda eneo la Kigamboni leo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad