HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 22, 2014

Wafugaji kigamboni wakabidhiwa mikopo ya N’gombe wa maziwa 83

Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dr. Titus Kamani, amekabidhi mikopo ya Ng’ombe wa maziwa themanini na tatu (83) kwa kikundi cha wafugaji cha Somangira walioko Kigamboni wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam.

Ng’ombe hao ambao wamenunuliwa kwa mkopo uliotolewa na Covenant Bank wana uwezo wa kuzalisha maziwa zaidi ya Lita 20 kwa siku. Akizungumza na wakazi wa eneo hilo Waziri Kamani ametanabaisha  kuwa mikopo ya aina hiyo italeta mapinduzi makubwa katika sekta ya mifugo.

“Kitendo cha kukabidhiwa Ng’ombe kwa kikundi cha wafugaji wadogo wa Somangira kinafanyika kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu hususan katika sekta ya mifugo, Mikopo ya aina hii imekuwa ikitolewa i kwa Ranchi za taifa lakini haikuwahi kutolewa kwa wafugaji wadogo wadogo” alisema Dk. Kamani na kuongeza kuwa,.

“Hatua hii ni ya kupongezwa sana hasa kutokana na Uhitaji mkubwa wa Maziwa uliopo nchini kwa sasa, ambapo kama nchi tunatakiwa kuzalisha lita bilioni 9 za maziwa kwa siku ili kuwatosheleza watu wetu lakini kwa sasa tuna uwezo wa kuzalisha lita bilioni mbili tu, Hivyo ninaomba benki hii kwa kushirikiana na wadau wengine waendelee kutoa mikopo hii kwa vikundi vingine ili kuongeza uzalishaji”. Alisema.

Aidha, Dr Kamani aliwataka wana kikundi hao kuhakikisha wanawatumia ng’ombe hao katika kujipatia kipato na kurudisha mikopo hiyo kwa wakati ili kuwezesha vikundi vingine kukopa kupitia marejesho hayo.

Awali, akizungumza na wananchi wa Somangira Mkurugenzi wa Covenant Bank, Bibi Sabetha Mwambenja amesema ng’ombe hao 83 wamekatiwa bima hivyo endapo gg’ombe hao watakufa au kupatwa na tatizo lolote kampuni ya bima itachukua jukumu la kumlipia mkopo wake mfugaji aliyeathirika.

“Licha ya kutoa mikopo ya ng’ombe kwa hawa wakulima, Covenant Bank, tumekwenda mbali zaidi kwa kuwawezesha wakulima hawa kupata mafunzo ya ufugaji wa kisasa wa Ng’ombe wa Maziwa kutoka kwa wataalam wa bodi ya maziwa na tayari mabanda yamekaguliwa na kujiridhisha kuwa sasa watakuwa mahali salama’’, Alisema.

Kwa Upande wake Katibu wa Kikundi  hicho Bi. Getrude Mpelembe, aliishukuru Benki hiyo huku akitoa wito kwa Serikali kuboresha miundombinu kwa wafugaji wadogo kwa kuwapatia wataalam wa kutosha na kutafuta soko la maziwa la uhakika.
Mkurugenzi wa Covenant Bank, Sabetha Mwambenja, akimpokea Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dr, Titus Kamani, wakati akiwasili katika hafla ya kukabidhi Ng’ombe 83 wa Maziwa kwa wafugaji wadogo wa Kikundi cha Somangira walioko Kigamboni Jijini Dar es Salaam, Ng’ombe hao wamenunuliwa kwa Mkopo kutoka Covenant Bank.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dr. Titus Kamani, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Somangira, Kigamboni Jijini Dar es Salaam katika hafla ya kukabidhi Ng’ombe 83 wa maziwa kwa kikundi wafugaji wadogo wa kijiji hicho Ng’ombe hao wamenunuliwa kwa Mkopo kutoka Covenant Bank. Pamoja nae katika Picha ni Mkurugenzi wa Covenant Bank. Sabetha Mwambenja.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dr. Titus Kamani, akikamua Maziwa kutoka kwa moja ya Ng’ombe 83 wa Maziwa, punde baada ya Kuwakabidhi kwa wafugaji wa kikundi cha Somangira – Kigamboni jijini Dar es Salaam, wanaoshuhudia ni Mratibu wa Kikundi hicho Bibi. Getrude Mpelembe(kushoto) Mkurugenzi wa Covenant Bank. Bibi Sabetha Mwambenja (Katikati) na Mwenyekiti wa Wajasiriamali wasio katika Sekta Rasmi, Dauda Salmin.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dr. Titus Kamani, akikabidhi moja ya Ng’ombe 83 wa Maziwa, kwa Bibi. Robi Chacha ambaye ni miongoni mwa wanakikundi 83 waliokabidhiwa Ng’ombe hao ambao wamenunuliwa kwa Mkopo na Covenant Bank. Wanaoshuhudia ni Mkurugenzi wa Covenant Bank. Sabetha Mwambenja, (Mwenye miwani katikati) na Mwenyekiti wa Wajasiriamali wasio katika Sekta Rasmi Dauda Salmin.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad