HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 29, 2014

NCHI 188 ZAPIGA KURA YA NDIYO YA KUTAKA CUBA IONDOLEWE VIKWAZO

Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan Mwinyi akizungumza muda mfupi kabla wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hawajapigia kura ya kutaka vikwazo vya kiuchumi, kibiashara na kifedha ambavyo Marekani imeiwekea Cuba viondolowe. nchi 188 zilipiga kura ya ndiyo, mbili zilipiga kura ya hapana na tatu zilipiga kura ya kutofungamana na upande wowote.

Na Mwandishi Maalum , New York

Kwa mwaka wa 23 sasa hapo jana ( Jumanne ) Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wamepigia kura Azimio linaloitaka Marekani iondoe vikwazo vya kiuchumi, kibiashara na kifedha dhidi ya Cuba.

Katika upigaji kura huo , nchi 188 ikiwamo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilipiga kura ya ndiyo Azimio hilo ambalo liliwasilishwa mbele ya wajumbe na Waziri wa Mamb ya Nje wa Cuba, Bw. Bruno Rodriquez Parrilla Marekani na Israel zenyewe zilipiga kura ya hapana, huku Micronesia, Marshall Islands na Palau wakipiga kura ya kutoegemea upande wowote ( abstentions).

Akizungumza kabla ya upigaji kura huo kufanyika, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Ramadhan Mwinyi aliungana na wazungumzaji wengine katika kuitaka Marekani na Cuba kumaliza tofauti zao za kidiplomasia ili waweze kushirikiana na nchi nyingine katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazomkabili mwanadamu.

Akasema dunia imeshuhudia namna gani mataifa mengi yalivyojitoa muhanga zikiwamo Cuba na Marekani ambapo wamepeleka wataalamu wao wa afya, wanajeshi na vifaa ili kuukabili ugonjwa wa Ebola katika nchi za Liberia, Sierra Leone na Guinea ambazo zimeathirika vibaya kwa ugonjwa huu.

Akasisitiza kuwa mlipuko huo wa Ebola umethihirisha namna gani mataifa yanavyoweza kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja na kwamba mataifa yanatakiwa kujenga mshikamano imara dhidi ya maadui wa binadamu na siyo kupingana wenyewe kwa wenyewe.

Balozi Mwinyi akaongeza kuwa Tanzania ambayo ni nchi rafiki kwa Marekani na Cuba, kwa mara nyingine inasikitika kusimama na kuzungumzia kuhusu vikwazo hivyo ambavyo licha ya maazimio mengi kupitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Bado vikwazo vinaendelea.

Vile vile Balozi Mwinyi amesema hali ya kuendelea kwa vikwazo hivyo kunasikitisha kutokana na sababu kuu mbili za msingi. Kwanza kuchelewa kulipatia ufumbuzi tatizo hilo kunadhoofisha hadhi ya Umoja wa Mataifa, chombo chenye dhamana ya kuhifadhi Amani na usalama wa kimataifa, kuhuisha haki za binadamu, uchumi na ustawi wa wote.

Akasema inaposhindikana kutekelezwa kwa maazimio yanayopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni kushindwa kwa wanachama wote. Sababu ya pili ambayo amesema inasikitisha ni kuona kuwa Nchi ambayo ilikuwa mwazilishi wa Umoja wa Mataifa ( Marekani) inaendelea kupuuza wito ambao umekuwa ukitolewa mara kwa mara, wito unaotolewa wanachama wa Umoja wa Mataifa wa kutaka kusitishwa mara moja na bila masharti yoyote vikwazo dhidi ya Cuba.

“ Tatizo hili ( vikwazo) linaweza kuwa ni la kati ya nchi hizo mbili. Lakini kuendelea kwake na muda mrefu kunavuka mipaka ya nchi hizi mbili” akasema Balozi Mwinyi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad