HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 22, 2014

MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA MABALOZI WA NORWAY NA RWANDA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo amekutana na mabalozi wa Norway na Balozi mteule wa Tanzania nchini Rwanda na kufanya nao mazungumzo ofisini kwake ikulu jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Norway nchini Tanzania mheshimiwa Hanne Marie Kaarstad ndiye alikuwa wa kwanza kufanya mazungumzo na mheshimiwa Makamu wa Rais ambapo licha ya kufika kujitambulisha alimueleza mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa atajitahidi kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizi mbili katika kipindi chake kama Balozi na kwamba Tanzania ni nchi rafiki kwa Norway na akasisitiza kuzidi kuimarisha uhusiano hasa katika masuala ya utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake mheshimiwa Makamu wa Rais alimuelezea Balozi Hanne kuwa, Tanzania inajivunia uhusiano wake na Norway na kwamba uhusiano huo kwa sasa unazidi kuimarika na tena Tanzania inategemea kujifunza mengi toka Norway kutokana na nchi hiyo kuwa miongoni mwa nchi zenye teknolojia ya juu katika masuala ya gesi na mafuta.

Balozi Hanne ambaye aliwahi kufanya kazi nchini Tanzania pia alionesha kufurahishwa kwake na maendeleo ambayo Tanzania inapiga na akafafanua kuwa mji wa Dar es Salaam ni kiashiria kimojawapo kinachoonesha wazi kuwa Tanzania inakuwa kwa kasi.

Pia, Mheshimiwa Makamu wa Rais alimpokea Balozi Ali Said Siwa aliyepangiwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Rwanda na akamtaka Balozi huyo kuhakikisha anasaidia mahusiano baina ya nchi zetui kuzidi kuimarika huku akimsisitizia kuhusu uhusiano wetu kama majirani na pia wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Balozi Siwa alitumia nafasi hiyo kumshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa uteuzi wake na akaahidi kuiwakilisha vema Tanzania nchini Rwanda.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Hanne Marie Kaarstad, wakati alipofika ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Septemba 22, 2014 kwa mazungumzo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Hanne Marie Kaarstad, (wa pili kulia) na ujumbe wake baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Septemba 22, 2014.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkaribisha Balozi wa Tanzania, nchini Rwanda, Mhe. Ali Said Siwa, wakati alipofika ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Septemba 22, 2014.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Balozi wa Tanzania, nchini Rwanda, Mhe. Ali Said Siwa, leo Septemba 22, 2014. Picha na OMR.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad