HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 23, 2014

Wizara ya Nishati na Madini kuanzisha Mpango wa Taifa wa Matumizi Bora ya Nishati

 Na Greyson Mwase, Morogoro
Wizara ya nishati na madini inatarajia kuanzisha mpango wa taifa wa matumizi bora ya nishati  unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mara baada ya maandalizi yake kukamilika.

Akizungumza katika  kongamano la mabadiliko ya tabianchi lililokutanisha wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam linaloendelea mjini Morogoro, Mhandisi Nyaso Makwaya kutoka Idara ya Nishati, Wizara ya Nishati na Madini alisema kuwa mpango huo uko katika hatua za mwisho za ukamilishwaji wake.

Mhandisi Makwaya alisema kuwa maandalizi ya mpango huo yalianza mwaka 2013 na kuongeza kuwa lengo la mpango huu ni kuweka malengo ya kitaifa kwa kila sekta kwa ajili ya matumizi bora ya nishati, kuzichanganua changamoto zilizopo za matumizi bora ya nishati na kuzitafutia utatuzi na kuandaa miradi ya matumizi bora ya nishati.

“ Nishati ya umeme ni muhimu sehemu yoyote, inahitaji usimamizi  bora hivyo mpango huu  unalenga kuboresha matumizi ya nishati katika sekta zote nchini, iwe viwanda, kilimo, ujenzi,mawasiliano n.k, mpango huu unatoa dira sahihi kwa kila sekta” Alisema Mhandisi  Makwaya
Mhandisi Makwaya aliongeza kuwa  mpango huu utapelekea  uanzishwaji wa  sheria na kanuni katika usimamizi wa matumizi bora ya nishati.

Aliongeza kuwa  wadau na watekelezaji wakuu wa mpango huo ni Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Shirika la Taifa la Viwango (TBS) ambao watajengewa uwezo na mradi huu.

Akizungumzia changamoto zilizopo katika usimamizi wa matumizi  bora ya nishati   Mhandisi Makwaya alieleza kuwa  ni kutokuwepo kwa kanuni  zinazosimamia matumizi  bora ya nishati  katika ujenzi  na matokeo yake ni wajenzi kujenga majengo  yasiyokuwa na uwiano kati ya ukubwa wake na kiasi cha nishati ya umeme  kinachohitajika.

Mhandisi Makwaya alisisitiza kuwa  changamoto hiyo ilipelekea Wizara kubuni mkakati huo ambao utaisaidia nchi kuokoa kiasi cha nishati kinachopotea na kuongeza kuwa katika utekelezaji wa mpango huo  elimu kwa umma itatolewa ili wananchi wawe na uelewa wa kusimamia vyema matumizi bora ya nishati .

“Wananchi wengi hususani wafanyakazi maofisini na viwandani hawana uelewa juu ya matumizi sahihi ya nishati ya umeme, mpango huu utakuwa ni mkombozi na hii itachangia uchumi wa nchi kukua kwa haraka kwa kuokoa gharama zisizo za lazima. “ Alisisitiza Mhandisi  Makwaya
Mtaalamu kutoka Idara ya Nishati iliyopo chini ya Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Nyaso Makwaya akisisitiza jambo wakati alipokuwa  akiwasilisha mada kuhusiana na mikakati ya Wizara katika kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad